15. Siku zile akasimama Petro kati ya hao ndugu (jumla ya majina ilipata mia na ishirini), akasema,
16. Ndugu, ilipasa andiko litimizwe, alilolinena Roho Mtakatifu zamani kwa kinywa cha Daudi, katika habari za Yuda aliyewaongoza wao waliomkamata Yesu;
17. kwa sababu alikuwa amehesabiwa pamoja na sisi, akapata sehemu ya huduma hii.
18. (Basi mtu huyu alinunua konde kwa ijara ya udhalimu; akaanguka kwa kasi akapasuka matumbo yake yote yakatoka.
19. Ikajulikana na watu wote wakaao Yerusalemu; hata konde lile likaitwa kwa lugha yao Akeldama, maana yake, konde la damu.)
20. Kwa maana imeandikwa katika chuo cha Zaburi,Kikao chake na kiwe ukiwa,Wala asiwepo mtu mwenye kukaa humo;tena,Usimamizi wake autwae mwingine.
21. Basi katika watu waliofuatana nasi wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiingia na kutoka kwetu,
22. kuanza tangu ubatizo wa Yohana, hata siku ile alipochukuliwa kwetu kwenda juu, inapasa mmoja wao awe shahidi wa kufufuka kwake pamoja nasi.
23. Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya.
24. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili,