Lk. 9:9-20 Swahili Union Version (SUV)

9. Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona.

10. Basi wale mitume waliporudi walimweleza mambo yote waliyoyatenda; akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida.

11. Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa.

12. Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu.

13. Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula.

14. Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini.

15. Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote.

16. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano.

17. Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili.

18. Ikawa alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani?

19. Wakamjibu wakisema, Yohana Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka.

20. Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu.

Lk. 9