1. Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.
2. Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa.
3. Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili.
4. Na nyumba yo yote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke mjini.
5. Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo, yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao.
6. Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri injili, na kupoza watu kila mahali.
7. Na Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu,
8. na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka.
9. Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona.
10. Basi wale mitume waliporudi walimweleza mambo yote waliyoyatenda; akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida.