46. Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka.
47. Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara.
48. Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani.
49. Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia, Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu.
50. Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa.
51. Alipofika nyumbani hakuacha mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye.
52. Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu.
53. Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa.
54. Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka.
55. Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula.
56. Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini akawakataza wasimwambie mtu lililotukia.