Lk. 7:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. maana, analipenda taifa letu, naye alitujengea sinagogi.

6. Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu;

7. kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona.

8. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.

9. Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii.

10. Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima.

11. Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa.

12. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye.

13. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie.

14. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka.

15. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake.

16. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.

17. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.

18. Wanafunzi wa Yohana wakamletea habari za hayo yote.

Lk. 7