Lk. 6:11-27 Swahili Union Version (SUV)

11. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.

12. Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu.

13. Hata kulipokuwa mchana aliwaita wanafunzi wake; akachagua kumi na wawili miongoni mwao, ambao aliwaita Mitume;

14. Simoni, aliyemwita jina la pili Petro, na Andrea nduguye, na Yakobo na Yohana, na Filipo na Bartolomayo,

15. na Mathayo na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Simoni aitwaye Zelote,

16. na Yuda wa Yakobo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyekuwa msaliti.

17. Akashuka pamoja nao, akasimama mahali tambarare, pamoja na wanafunzi wake wengi, na makutano makubwa ya watu waliotoka Uyahudi wote na Yerusalemu, na pwani ya Tiro na Sidoni; waliokuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao;

18. na wale waliosumbuliwa na pepo wachafu; waliponywa.

19. Na makutano yote walikuwa wakitaka kumgusa, kwa sababu uweza ulikuwa ukimtoka ukiwaponya wote.

20. Akainua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.

21. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi mliao sasa, kwa sababu mtacheka.

22. Heri ninyi watu watakapowachukia, na kuwatenga, na kuwashutumu, na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

23. Furahiwani siku ile na kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni, maana, baba zao waliwatenda manabii vivyo hivyo.

24. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha kuipata.

25. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia.

26. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.

27. Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi,

Lk. 6