Lk. 5:22-35 Swahili Union Version (SUV)

22. Na Yesu alijua hoja zao, akajibu akawaambia, Mnahojiana nini mioyoni mwenu?

23. Lililo jepesi ni lipi? Kusema, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, uende?

24. Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia, Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako.

25. Mara hiyo akasimama mbele yao, akajitwika kile alichokilalia, akaenda zake nyumbani kwake, huku akimtukuza Mungu.

26. Ushangao ukawashika wote, wakamtukuza Mungu; wakajaa hofu, wakisema, Leo tumeona mambo ya ajabu.

27. Baada ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate.

28. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata.

29. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao.

30. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?

31. Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi.

32. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.

33. Nao wakamwambia, Wanafunzi wa Yohana hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa!

34. Lakini Yesu akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao?

35. Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile.

Lk. 5