Lk. 3:5-14 Swahili Union Version (SUV)

5. Kila bonde litajazwa,Na kila mlima na kilima kitashushwa;Palipopotoka patakuwa pamenyoka,Na palipoparuza patalainishwa;

6. Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.

7. Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8. Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.

9. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

10. Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi?

11. Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo.

12. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi?

13. Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.

14. Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.

Lk. 3