8. Wakayakumbuka maneno yake.
9. Wakaondoka kaburini, wakarudi; wakawaarifu wale kumi na mmoja na wengine wote habari za mambo hayo yote.
10. Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao;
11. hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo.
12. Maneno yao yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki. Lakini Petro aliondoka akaenda mbio hata kaburini, akainama akachungulia ndani, akaviona vile vitambaa vya sanda tu; akaenda zake akiyastaajabia yaliyotukia.
13. Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.
14. Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.
15. Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.
16. Macho yao yakafumbwa wasimtambue.
17. Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.
18. Akajibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?
19. Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;
20. tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.
21. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;