Lk. 24:33-44 Swahili Union Version (SUV)

33. Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao,

34. wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni.

35. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.

36. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.

37. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho.

38. Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?

39. Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.

40. Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake.

41. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, Mna chakula cho chote hapa?

42. Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa.

43. Akakitwaa, akala mbele yao.

44. Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii na Zaburi.

Lk. 24