Lk. 24:29-39 Swahili Union Version (SUV)

29. Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.

30. Ikawa alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.

31. Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.

32. Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?

33. Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao,

34. wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni.

35. Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.

36. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.

37. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho.

38. Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?

39. Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.

Lk. 24