40. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?
41. Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.
42. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.
43. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.
44. Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,
45. jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.
46. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.
47. Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.
48. Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua.
49. Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.
50. Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki;
51. (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu;
52. mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu.
53. Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake.
54. Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.
55. Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa.