Lk. 23:34-42 Swahili Union Version (SUV)

34. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.

35. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.

36. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,

37. huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.

38. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

39. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

40. Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41. Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.

42. Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.

Lk. 23