Lk. 23:21-39 Swahili Union Version (SUV)

21. Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe.

22. Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.

23. Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda.

24. Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike.

25. Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.

26. Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.

27. Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.

28. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.

29. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha.

30. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.

31. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

32. Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.

33. Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto.

34. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.

35. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.

36. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,

37. huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.

38. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

39. Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

Lk. 23