Lk. 22:35-46 Swahili Union Version (SUV)

35. Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!

36. Akawaambia, Lakini sasa mwenye mfuko na auchukue, na mkoba vivyo hivyo; naye asiye na upanga, na auze joho yake akanunue.

37. Kwa kuwa nawaambia, hayo yaliyoandikwa hayana budi kutimizwa kwangu; ya kuwa, Alihesabiwa pamoja na wahalifu. Kwa sababu yanipasayo yanao mwisho wake.

38. Wakasema, Bwana, tazama, hapa pana panga mbili. Akawaambia, Basi.

39. Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.

40. Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni.

41. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba,

42. akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [

43. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.

44. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]

45. Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni.

46. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.

Lk. 22