11. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu?
12. Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo.
13. Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka.
14. Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye.
15. Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu;
16. kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu.
17. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi;
18. Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja.
19. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.
20. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]
21. Walakini, tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani,
22. Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye!
23. Wakaanza kuulizana wao kwa wao, ni yupi miongoni mwao atakayelitenda jambo hilo.
24. Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa.
25. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili;
26. lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.
27. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.
28. Nanyi ndinyi mliodumu pamoja nami katika majaribu yangu.
29. Nami nawawekea ninyi ufalme, kama vile Baba yangu alivyoniwekea mimi;