10. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme;
11. kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
12. Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu.
13. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu.
14. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu;
15. kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.
16. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu.
17. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu.
18. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu.
19. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.
20. Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.
21. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.
22. Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.
23. Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.
24. Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.
25. Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake;
26. watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika.