Lk. 20:7-15 Swahili Union Version (SUV)

7. Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka.

8. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.

9. Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu.

10. Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu.

11. Akatuma na mtumwa mwingine. Wakampiga huyu naye, wakamwaibisha wakamfukuza mikono mitupu.

12. Akamtuma na wa tatu; huyu naye wakamtia jeraha, wakamtupa nje.

13. Basi, bwana wa shamba la mizabibu alisema, Nifanyeje? Nitamtuma mwanangu, mpendwa wangu; yamkini watamheshimu yeye.

14. Lakini, wale wakulima walipomwona, walishauriana wao kwa wao, wakisema, Huyu ndiye mrithi; haya, na tumwue, ili urithi uwe wetu.

15. Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi, bwana wa shamba la mizabibu atawatendeje?

Lk. 20