1. Ikawa siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni, na kuihubiri habari njema, wakuu wa makuhani na waandishi pamoja na wazee walimtokea ghafula;
2. wakamwambia, wakisema, Tuambie, unatenda mambo hayo kwa mamlaka gani? Tena, ni nani aliyekupa mamlaka hii?
3. Akajibu akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja; niambieni,
4. Ubatizo wa Yohana, je! Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?
5. Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema ulitoka mbinguni, atasema, Basi, mbona hamkumwamini?
6. Na tukisema ulitoka kwa wanadamu, watu wote watatupiga kwa mawe, kwa kuwa wamemkubali Yohana kuwa ni nabii.
7. Wakajibu, kwamba, Hatujui ulikotoka.
8. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.
9. Akaanza kuwaambia watu mfano huu; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu; akapangisha wakulima, akaenda akakaa katika nchi nyingine muda mrefu.
10. Na wakati wa mavuno alituma mtumwa kwa wale wakulima ili wampe baadhi ya matunda ya mizabibu; wakulima wakampiga wakamfukuza mikono mitupu.