38. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
39. Basi, walipokwisha kuyatimiza yote kama yalivyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya mpaka mjini kwao, Nazareti.
40. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
41. Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.
42. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;
43. na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.
44. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;
45. na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.