Lk. 2:14-31 Swahili Union Version (SUV)

14. Atukuzwe Mungu juu mbinguni,Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.

15. Ikawa, malaika hao walipoondoka kwenda zao mbinguni, wale wachungaji waliambiana, Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukalione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana.

16. Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelala horini.

17. Walipomwona wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto.

18. Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.

19. Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.

20. Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.

21. Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.

22. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana,

23. (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),

24. wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili.

25. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.

26. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.

27. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria,

28. yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,

29. Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako,Kwa amani, kama ulivyosema;

30. Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,

31. Uliouweka tayari machoni pa watu wote;

Lk. 2