Lk. 19:21-38 Swahili Union Version (SUV)

21. Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

22. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

23. basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

24. Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

25. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

26. Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho.

27. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.

28. Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

29. Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi,

30. akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa.

31. Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.

32. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.

33. Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda?

34. Wakasema, Bwana ana haja naye.

35. Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu.

36. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani.

37. Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,

38. wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.

Lk. 19