Lk. 13:29-35 Swahili Union Version (SUV)

29. Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu.

30. Na tazama, wako walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, na wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.

31. Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua.

32. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.

33. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.

34. Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala hamkutaka.

35. Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.

Lk. 13