17. Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.
18. Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini?
19. Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.
20. Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu?
21. Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.
22. Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu.
23. Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia,
24. Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.