13. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.
14. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.
15. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng’ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha?
16. Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato?
17. Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.
18. Kisha alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini?
19. Umefanana na punje ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake.
20. Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu?
21. Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.
22. Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu.