Lk. 1:9-19 Swahili Union Version (SUV)

9. kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.

10. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.

11. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.

12. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.

13. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.

14. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.

15. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.

16. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.

17. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.

18. Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi.

19. Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.

Lk. 1