7. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.
8. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,
9. kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.
10. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.
11. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.
12. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
13. Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.
14. Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.
15. Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.
16. Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.
17. Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.