27. kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
28. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.
29. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?
30. Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.
31. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.
32. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.
33. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.
34. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?
35. Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.
36. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa;
37. kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.
38. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
39. Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,
40. akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti.
41. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu;
42. akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
43. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?
44. Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu.
45. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.
46. Mariamu akasema,Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
47. Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu;