21. Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni.
22. Alipotoka hali hawezi kusema nao, walitambua ya kuwa ameona maono ndani ya hekalu, naye aliendelea kuwaashiria akakaa bubu.
23. Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake.
24. Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema,
25. Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.
26. Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,
27. kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
28. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.
29. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?
30. Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu.
31. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.
32. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake.