1. Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu,
2. kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo,
3. nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,
4. upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.
5. Zamani za Herode, mfalme wa Uyahudi, palikuwa na kuhani mmoja, jina lake Zakaria, wa zamu ya Abiya, na mkewe alikuwa mmojawapo wa uzao wa Haruni, jina lake Elisabeti.
6. Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama.
7. Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana.
8. Basi ikawa, alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,
9. kama ilivyokuwa desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.
10. Na makutano yote ya watu walikuwa wakisali nje saa ya kufukiza uvumba.
11. Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia.
12. Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.