16. Lakini kwamba hii sadaka ya matoleo yake ni nadhiri, au sadaka ya hiari, italiwa siku hiyo aliyoileta sadaka yake; kisha siku ya pili yake kitakachosalia kitaliwa;
17. lakini hicho kitakachosalia, katika hizo nyama za sadaka, hata siku ya tatu kitachomwa moto.
18. Tena kama nyama yo yote katika hiyo dhabihu yake ya sadaka za amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitahesabiwa kwake huyo mwenye kuisongeza; itakuwa ni machukizo, na mtu atakayeila atachukua uovu wake.
19. Tena nyama itakayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa; itachomwa moto. Na katika hiyo nyama nyingine, kila mtu aliye safi ana ruhusa kuila;
20. lakini mtu huyo atakayekula katika nyama ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, na unajisi wake akiwa nao juu yake, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
21. Kisha mtu awaye yote atakapogusa kitu cho chote kilicho najisi, uchafu wa binadamu, au mnyama aliye najisi, au machukizo yo yote yaliyo najisi, kisha akala nyama ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
22. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
23. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Msile mafuta yo yote, ya ng’ombe, wala ya kondoo, wala ya mbuzi.
24. Tena mafuta ya mnyama afaye mwenyewe, na mafuta ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, mna ruhusa kuyatumia kwa ajili ya matumizi mengine; lakini msiyale kabisa.
25. Kwani huyo mtu atakayekula mafuta ya mnyama, ambaye ni katika wanyama ambao watu husongeza sadaka kwa BWANA kwa moto, mtu huyo atakayekula mafuta hayo atakatiliwa mbali na watu wake.
26. Tena msiile damu yo yote, ama ya ndege, ama ya mnyama, katika nyumba zenu zote.