10. Na kila sadaka ya unga, kama umeandaliwa na mafuta, au kama ni mkavu, watautwaa wana wote wa Haruni kuutumia, kila mtu sawasawa.
11. Na sheria ya matoleo ya sadaka za amani, atakazosongeza mtu kwa BWANA, ni hii.
12. Kwamba aitoa kwa ajili ya shukrani, ndipo atakaposongeza pamoja na hiyo sadaka ya shukrani mikate isiyotiwa chachu, iliyoandaliwa na mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa iliyopakwa mafuta, na mikate ya unga mwembamba uliolowama mafuta.
13. Ataleta matoleo yake, pamoja na mikate iliyotiwa chachu, na pamoja na sadaka zake za amani, kwa ajili ya shukrani.
14. Na katika hayo atasongeza kimoja katika kila toleo kiwe sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA; itakuwa ni ya kuhani atakayeinyunyiza hiyo damu ya sadaka za amani.
15. Na hiyo nyama ya sadaka zake za amani zilizochinjwa kwa ajili ya shukrani italiwa siku iyo hiyo ya matoleo yake; asisaze yo yote hata asubuhi.
16. Lakini kwamba hii sadaka ya matoleo yake ni nadhiri, au sadaka ya hiari, italiwa siku hiyo aliyoileta sadaka yake; kisha siku ya pili yake kitakachosalia kitaliwa;
17. lakini hicho kitakachosalia, katika hizo nyama za sadaka, hata siku ya tatu kitachomwa moto.
18. Tena kama nyama yo yote katika hiyo dhabihu yake ya sadaka za amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitahesabiwa kwake huyo mwenye kuisongeza; itakuwa ni machukizo, na mtu atakayeila atachukua uovu wake.
19. Tena nyama itakayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa; itachomwa moto. Na katika hiyo nyama nyingine, kila mtu aliye safi ana ruhusa kuila;
20. lakini mtu huyo atakayekula katika nyama ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, na unajisi wake akiwa nao juu yake, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
21. Kisha mtu awaye yote atakapogusa kitu cho chote kilicho najisi, uchafu wa binadamu, au mnyama aliye najisi, au machukizo yo yote yaliyo najisi, kisha akala nyama ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo ni za BWANA, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
22. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
23. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Msile mafuta yo yote, ya ng’ombe, wala ya kondoo, wala ya mbuzi.