Law. 6:7-19 Swahili Union Version (SUV)

7. na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.

8. BWANA akanena na Musa na kumwambia,

9. Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.

10. Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.

11. Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi.

12. Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.

13. Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.

14. Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za BWANA, mbele ya madhabahu.

15. Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa BWANA.

16. Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula.

17. Hautaokwa na chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia.

18. Kila mwana mume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya BWANA yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu awaye yote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu

19. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

Law. 6