Law. 4:5-18 Swahili Union Version (SUV)

5. Kisha huyo kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa baadhi ya damu ya huyo ng’ombe, na kuileta ndani ya hiyo hema ya kukutania;

6. kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza damu mbele ya BWANA mara saba, mbele ya pazia la mahali patakatifu.

7. Kisha kuhani atatia baadhi ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba mzuri mbele ya BWANA iliyo ndani ya hema ya kukutania; kisha damu yote ya huyo ng’ombe ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyoko mlangoni pa hema ya kukutania.

8. Kisha mafuta yote ya huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi atayaondoa; mafuta yote yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,

9. na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo, hayo yote atayaondoa,

10. vile vile kama yanavyoondolewa katika ng’ombe wa kuchinjwa kwa sadaka za amani; kisha huyo kuhani atayateketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.

11. Kisha ngozi yake ng’ombe, na nyama yake yote, pamoja na kichwa chake, na pamoja na miguu yake, na matumbo yake, na mavi yake,

12. maana, huyo ng’ombe mzima atamchukua nje ya marago hata mahali safi, hapo wamwagapo majivu, naye atamchoma moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo majivu yamwagwapo.

13. Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na BWANA, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia;

14. hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng’ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania.

15. Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng’ombe mbele za BWANA;

16. kisha ng’ombe atachinjwa mbele za BWANA. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa katika damu ya huyo ng’ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania;

17. kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za BWANA, mbele ya pazia mara saba.

18. Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za BWANA, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania.

Law. 4