Law. 4:13-23 Swahili Union Version (SUV)

13. Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na BWANA, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia;

14. hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng’ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania.

15. Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng’ombe mbele za BWANA;

16. kisha ng’ombe atachinjwa mbele za BWANA. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa katika damu ya huyo ng’ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania;

17. kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za BWANA, mbele ya pazia mara saba.

18. Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za BWANA, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania.

19. Kisha atayaondoa mafuta yake yote na kuyateketeza juu ya madhabahu.

20. Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng’ombe; kama alivyomfanyia huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu vivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa.

21. Kisha atamchukua huyo ng’ombe nje ya marago, na kumchoma moto vile vile kama alivyomchoma moto ng’ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano.

22. Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lo lote katika hayo ambayo BWANA, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia;

23. akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi awe matoleo yake, mume, mkamilifu;

Law. 4