1. BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2. Haya, nena na wana wa Israeli, uwaambie, Kama mtu ye yote akifanya dhambi pasipo kukusudia, katika neno lo lote ambalo BWANA amelizuilia lisifanywe, na kutenda neno lo lote la maneno hayo;
3. kama kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi, hata analeta hatia juu ya watu; ndipo na atoe kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya, na kumsongeza kwa BWANA ng’ombe mume mchanga mkamilifu, kuwa ni sadaka ya dhambi.
4. Naye atamleta huyo ng’ombe na kumweka mlangoni pa hiyo hema ya kukutania, mbele za BWANA; naye ataweka mkono wake kichwani mwake ng’ombe, na kumchinja huyo ng’ombe mbele za BWANA.
5. Kisha huyo kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa baadhi ya damu ya huyo ng’ombe, na kuileta ndani ya hiyo hema ya kukutania;
6. kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza damu mbele ya BWANA mara saba, mbele ya pazia la mahali patakatifu.
7. Kisha kuhani atatia baadhi ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba mzuri mbele ya BWANA iliyo ndani ya hema ya kukutania; kisha damu yote ya huyo ng’ombe ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyoko mlangoni pa hema ya kukutania.
8. Kisha mafuta yote ya huyo ng’ombe wa sadaka ya dhambi atayaondoa; mafuta yote yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
9. na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo, hayo yote atayaondoa,