27. Tena ikiwa baada ya hayo yote hamtaki kunisikiza, bali mwaenenda kwa kunishikia kinyume;
28. ndipo nami nitakwenda kwa kuwashikia ninyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba kwa dhambi zenu.
29. Nanyi mtakula nyama ya miili ya wana wenu, na nyama ya miili ya binti zenu mtaila.
30. Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia.
31. Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo.
32. Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia.
33. Nanyi nitawatapanya-tapanya katika mataifa, nami nitaufuta upanga nyuma yenu; na nchi yenu itakuwa ni ukiwa, na miji yenu maganjo.
34. Hapo ndipo nchi itakapozifurahia Sabato zake, wakati itakapokuwa hali ya ukiwa, nanyi mtakapokuwa katika nchi ya adui zenu; ndipo nchi itakapopumzika, na kuzifurahia Sabato zake.
35. Wakati wote itakapokuwa na ukiwa, itapumzika; ni hayo mapumziko ambayo haikuwa nayo katika Sabato zenu, hapo mlipokaa katika nchi hiyo.
36. Tena hao wa kwenu watakaobaki, nitawatilia woga mioyoni mwao, katika hizo nchi za adui zao; na sauti ya jani lililopeperushwa itawakimbiza; nao watakimbia, kama mtu akimbiavyo upanga; nao wataanguka hapo ambapo hapana afukuzaye.
37. Nao wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama mbele ya upanga, hapo ambapo hapana afukuzaye; wala hamtakuwa na nguvu za kusimama mbele ya adui zenu.
38. Nanyi mtaangamia kati ya mataifa, na nchi ya adui zenu itawameza.
39. Na watu wa kwenu watakaobaki watafifia kwa ajili ya uovu wao, katika hizo nchi za adui zenu; tena watafifia kwa ajili ya uovu wa baba zao, pamoja nao.