Law. 26:17-32 Swahili Union Version (SUV)

17. Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye.

18. Tena ikiwa baada ya hayo hamtaki kunisikiza, ndipo nitawaadhibu zaidi mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.

19. Nami nitakivunja kiburi cha uwezo wenu; nami nitazifanya mbingu zenu kuwa kama chuma, na nchi yenu kuwa kama shaba;

20. na nguvu zenu mtazitumia bure; kwa kuwa nchi yenu haitazaa mazao yake, wala miti ya nchi haitazaa matunda yake.

21. Nanyi ikiwa mwaenenda kinyume changu, wala hamtaki kunisikiza; nitaleta mapigo mara saba zaidi juu yenu, kama dhambi zenu zilivyo.

22. Nami nitaleta wanyama wakali kati yenu, ambao watawanyang’anya watoto wenu, na kuwaharibu wanyama wenu wa kufugwa, na kuwapunguza muwe wachache hesabu yenu; na njia zenu zitakuwa ni ukiwa.

23. Tena kama hamtaki kurejezwa upya kwangu mimi kwa mambo haya, bali mwaendelea kunishikia kinyume; ndipo mimi nami nitaendelea kuwashikia ninyi kinyume;

24. nami nitawapiga, naam mimi, mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.

25. Nami nitaleta upanga juu yenu, utakaopatiliza kisasi cha hilo agano; nanyi mtakutanishwa ndani ya miji yenu; nami nitaleta tauni kati yenu; nanyi mtatiwa mkononi mwa adui.

26. Hapo nitakapovunja tegemeo lenu la mkate, wanawake kumi wataoka mikate yenu katika tanuu moja, nao watawapa mikate yenu tena kwa kupima kwa mizani; nanyi mtakula, lakini hamtashiba.

27. Tena ikiwa baada ya hayo yote hamtaki kunisikiza, bali mwaenenda kwa kunishikia kinyume;

28. ndipo nami nitakwenda kwa kuwashikia ninyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba kwa dhambi zenu.

29. Nanyi mtakula nyama ya miili ya wana wenu, na nyama ya miili ya binti zenu mtaila.

30. Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia.

31. Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo.

32. Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia.

Law. 26