1. Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
2. Zishikeni Sabato zangu, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi BWANA.
3. Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya;
4. ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.
5. Tena kupura nafaka kwenu kutaendelea hata wakati wa kuvuna zabibu, na kuvuna zabibu kutaendelea hata wakati wa kupanda mbegu; nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, na kuketi katika nchi yenu salama.
6. Nami nitawapa amani katika nchi, tena mtalala wala hapana atakayewatia hofu; nami nitawakomesha wanyama wabaya katika nchi yenu, wala hautapita upanga katika nchi yenu.
7. Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga.
8. Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga.
9. Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza; nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi.
10. Nanyi mtakula akiba ya zamani mliyoiweka siku nyingi, tena hayo ya zamani mtayatoa, ili myaweke yaliyo mapya.
11. Nami nitaiweka maskani yangu kati yenu; wala roho yangu haitawachukia.
12. Nami nitakwenda kati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu.
13. Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ili msiwe watumwa wao; nami nimeivunja miti ya kongwa lenu, nikawaendesha mwende sawasawa.
14. Lakini msiponisikiza, wala hamtaki kuyafanya maagizo hayo yote;
15. nanyi mkizikataa amri zangu, na roho yenu ikichukia hukumu zangu, hata ikawa hamtaki kuyafanya maagizo yangu yote, bali mwalivunja agano langu;
16. mimi nami nitawatenda jambo hili; nitaamrisha uje juu yenu utisho, hata kifua kikuu na homa, zitakazoharibu macho yenu, na kuidhoofisha roho; nanyi mtapanda mbegu yenu bure, kwa kuwa adui zenu wataila.
17. Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye.
18. Tena ikiwa baada ya hayo hamtaki kunisikiza, ndipo nitawaadhibu zaidi mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
19. Nami nitakivunja kiburi cha uwezo wenu; nami nitazifanya mbingu zenu kuwa kama chuma, na nchi yenu kuwa kama shaba;
20. na nguvu zenu mtazitumia bure; kwa kuwa nchi yenu haitazaa mazao yake, wala miti ya nchi haitazaa matunda yake.