Law. 25:5-17 Swahili Union Version (SUV)

5. Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde; utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi.

6. Na hiyo Sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe;

7. na kwa hayawani wako, na kwa wanyama walio katika nchi yako; maongeo yote yatakuwa ni chakula chao.

8. Nawe utajihesabia Sabato saba za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda.

9. Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote.

10. Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu; nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake.

11. Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa.

12. Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani.

13. Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake.

14. Tena kama ukimwuzia jirani yako cho chote, au kununua cho chote mkononi mwa jirani yako, msidanganyane wenyewe kwa wenyewe;

15. kwa hesabu ya miaka iliyo baada ya yubile, ndivyo utakavyonunua kwa jirani yako, na kama hesabu ya miaka ya mavuno ndivyo atakavyokuuzia wewe.

16. Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo.

17. Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

Law. 25