41. ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake.
42. Kwa kuwa hao ni watumishi wangu, niliowaleta watoke nchi ya Misri; wasiuzwe mfano wa watumwa.
43. Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako.
44. Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi.
45. Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu.
46. Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; lakini msitawale kwa nguvu juu ya ndugu zenu, hao wana wa Israeli, wenyewe kwa wenyewe.
47. Tena kama mgeni au mtu akaaye nawe akitajirika, na nduguyo amekuwa maskini karibu naye, akajiuza kwa huyo mgeni, au kwa huyo akaaye kwako, au kwa ukoo wa jamaa ya huyo mgeni;
48. baada ya kuuzwa aweza kukombolewa; mtu mmoja miongoni mwa ndugu zake ana ruhusa kumkomboa;
49. au mjomba wake, au mwana wa mjomba wake, ana ruhusa ya kumkomboa, au mtu awaye yote aliye karibu naye wa jamaa yake, ana ruhusa ya kumkomboa; au kwamba yeye mwenyewe amepata mali, ana ruhusa ya kujikomboa mwenyewe.
50. Naye atafanya hesabu na huyo aliyemnunua, tangu mwaka huo aliojiuza hata mwaka wa yubile; na ile bei ya kuuzwa kwake itakuwa kama hesabu ya hiyo miaka ilivyo; atakuwa pamoja naye kama majira ya mtumishi aliyeajiriwa yalivyo.
51. Kwamba ikali imesalia miaka mingi, kama hesabu yake ilivyo ndivyo atakavyolipa bei ya ukombozi wake, katika hiyo fedha ambayo alinunuliwa kwayo.
52. Tena kwamba imesalia miaka michache tu hata mwaka wa yubile, ndipo atafanya hesabu naye, kama hesabu ya miaka yake ilivyo, ndivyo atakavyolipa tena bei ya ukombozi wake.
53. Kama mtumishi aliyeajiriwa mwaka hata mwaka, ndivyo atakavyokuwa pamoja naye; asitawale juu yake kwa nguvu mbele ya macho yako.
54. Tena kwamba hakukombolewa kwa njia hizi mojawapo, ndipo atatoka katika mwaka wa yubile, yeye, na watoto wake pamoja naye.
55. Kwa kuwa wana wa Israeli ni watumishi; ni watumishi wangu niliowaleta watoke katika nchi ya Misri; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.