Law. 25:22-39 Swahili Union Version (SUV)

22. Na mwaka wa nane mtapanda mbegu, na kuyala yale matunda, akiba hiyo ya zamani, hata mwaka wa kenda, hata matunda yake yatakapoletwa ndani, mtakula hiyo akiba ya zamani.

23. Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu.

24. Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu.

25. Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye.

26. Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa;

27. ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake.

28. Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake.

29. Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima.

30. Na kama haikukombolewa katika muda wa mwaka mzima, ndipo hiyo nyumba iliyo ndani ya mji wenye kuta itathibitishwa milele kuwa ya huyo aliyeinunua, katika vizazi vyake; nayo haitatoka katika yubile.

31. Lakini nyumba za vijiji, ambavyo havikuzingirwa na kuta, zitahesabiwa pamoja na mashamba ya nchi; nazo zina ruhusa ya kukombolewa, nazo zitatoka katika yubile.

32. Pamoja na hayo, miji ya Walawi, nyumba za miji ya milki yao, Walawi wana ruhusa ya kuzikomboa majira yo yote.

33. Tena kama mtu mmoja wa hao Walawi akikomboa, ndipo nyumba iliyouzwa, na mji wa milki yake, itatoka katika yubile; maana, hizo nyumba za miji ya Walawi ni milki yao kati ya wana wa Israeli.

34. Lakini konde la malisho ya miji yao lisiuzwe kwa kuwa ni milki yao ya daima.

35. Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri.

36. Usitake riba kwake wala faida, bali mche Mungu wako, ili ndugu yako akae nawe.

37. Usimpe fedha yako upate riba, wala usimpe vyakula vyako kwa kujitakia faida.

38. Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu.

39. Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa;

Law. 25