Law. 25:16-28 Swahili Union Version (SUV)

16. Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo.

17. Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

18. Kwa sababu hii zitendeni amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzifanya; nanyi mtakaa katika hiyo nchi salama.

19. Nayo nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba, na kuketi humo salama.

20. Na kama mkisema, Je! Mwaka wa saba tutakula nini? Angalieni hatutapanda mbegu, wala kukusanya maongeo yetu;

21. ndipo nitawaamria baraka yangu iwe juu yenu mwaka wa sita, nayo utazaa matunda hesabu ya miaka mitatu.

22. Na mwaka wa nane mtapanda mbegu, na kuyala yale matunda, akiba hiyo ya zamani, hata mwaka wa kenda, hata matunda yake yatakapoletwa ndani, mtakula hiyo akiba ya zamani.

23. Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu.

24. Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu.

25. Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye.

26. Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa;

27. ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake.

28. Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake.

Law. 25