1. Kisha BWANA akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia,
2. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika Sabato kwa ajili ya BWANA.
3. Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake;
4. lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa BWANA; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu.
5. Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde; utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi.
6. Na hiyo Sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe;
7. na kwa hayawani wako, na kwa wanyama walio katika nchi yako; maongeo yote yatakuwa ni chakula chao.