Law. 23:26-36 Swahili Union Version (SUV)

26. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

27. Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto.

28. Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za BWANA, Mungu wenu.

29. Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake.

30. Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake.

31. Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote.

32. Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.

33. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

34. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa BWANA.

35. Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.

36. Mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.

Law. 23