10. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;
11. naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.
12. Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.
13. Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.
14. Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote.
15. Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba;
16. hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea BWANA sadaka ya unga mpya.
17. Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa BWANA.
18. Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng’ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
19. Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani.
20. Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa BWANA, wawe wa huyo kuhani.
21. Nanyi mtapiga mbiu siku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yo yote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu.
22. Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
23. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
24. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu.