Law. 22:15-28 Swahili Union Version (SUV)

15. Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa BWANA;

16. hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye.

17. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

18. Nena na Haruni na wanawe, na wana wa israeli wote, uwaambie, Mtu ye yote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni nadhiri zao mojawapo, au kama ni sadaka yo yote ya hiari, watakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa;

19. ili mpate kukubaliwa, mtaleta mume mkamilifu, katika ng’ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi.

20. Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu.

21. Na mtu awaye yote atakayemtolea BWANA dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng’ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake cho chote.

22. Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea BWANA wanyama hao, wala msiwasongeze kwa BWANA kwa njia ya moto juu ya madhabahu.

23. Ng’ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa.

24. Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee BWANA; wala msifanye hivi katika nchi yenu.

25. Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao u ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu.

26. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

27. Hapo ng’ombe, au kondoo, au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa BWANA kwa njia ya moto.

28. Tena kama ni ng’ombe, au kama ni kondoo, msimchinje huyo na mwanawe wote wawili kwa siku moja.

Law. 22