Law. 22:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2. Nena na Haruni na wanawe, ili wajitenge wenyewe na vitu vitakatifu vya wana wa Israeli ambavyo wanitakasia mimi, tena kwamba wasilinajisi jina langu takatifu; mimi ndimi BWANA.

3. Waambie, Mtu ye yote wa kizazi chenu chote katika vizazi vyenu, atakayevikaribia vile vitu vitakatifu, ambavyo wana wa Israeli wamtakasia BWANA, naye ana unajisi, mtu huyo atakatiliwa mbali asiwe mbele zangu; mimi ndimi BWANA.

4. Mtu ye yote wa kizazi cha Haruni aliye mwenye ukoma, au mwenye kisonono; yeye asile katika vitu vitakatifu, hata atakapokuwa safi. Tena mtu awaye yote atakayekinusa kitu kilicho na unajisi kwa sababu ya wafu, au mtu ambaye shahawa humtoka;

5. au mtu amgusaye mnyama atambaaye, wa kumpatia unajisi, au kwamba amgusa mtu wa kumpatia unajisi, kwa unajisi wo wote alio nao;

6. huyo mtu atakayegusa kitu cho chote namna hiyo atakuwa najisi hata jioni, naye hatakula katika vitu vitakatifu, asipooga mwili wake majini.

7. Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake.

8. Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi BWANA.

9. Basi kwa hiyo watayashika mausia yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi BWANA niwatakasaye.

Law. 22