17. Tena mtu mume akimwoa umbu lake, binti ya baba yake, au binti ya mama yake, na kuuona utupu wake, na huyo mwanamke kauona utupu wake huyo mume; ni jambo la aibu; watakatiliwa mbali mbele ya macho ya wana wa watu wao; amefunua utupu wa umbu lake; naye atauchukua uovu wake.
18. Tena mtu mume akilala na mwanamke aliye na ugonjwa wake, na kufunua utupu wake; amelifunua jito la damu yake, naye mwanamke amefunua jito la damu yake; wote wawili watakatiliwa mbali na watu wao.
19. Usifunue utupu wa umbu la mama yako, wala umbu la baba yako; kwa kuwa huyo amefunua utupu wa jamaa yake ya karibu; watauchukua uovu wao.
20. Tena mtu mume akilala na mke wa mjomba wake, ameufunua utupu wa mjomba wake; watauchukua uovu wao; watakufa bila kuzaa mwana.
21. Tena mtu mume akimtwaa mke wa nduguye, ni uchafu; ameufunua utupu wa nduguye; hao watakuwa hawana wana.
22. Basi zishikeni amri zangu zote, na hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi kukaa, isiwatapike.
23. Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.