11. Sadaka ya unga iwayo yote itakayosongezwa kwa BWANA isitiwe chachu kabisa; kwa kuwa hamtateketeza chachu, wala asali iwayo yote, kuwa ni sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
12. Vitu hivyo mtavisongeza kwa BWANA kuwa ni malimbuko; lakini visifike juu ya madhabahu kuwa ni harufu ya kupendeza.
13. Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote.
14. Nawe kwamba wamtolea BWANA sadaka ya unga ya malimbuko, utatoa hiyo ngano katika masuke yake iliyochomwa motoni, ngano iliyopondwa ya masuke mabichi, ndiyo utakayoleta kuwa sadaka ya unga ya malimbuko yako.
15. Nawe utatia mafuta juu yake, na kuweka ubani juu yake; ni sadaka ya unga.
16. Huyo kuhani atauteketeza ukumbusho wake, yaani, sehemu ya ngano iliyopondwa ya hiyo sadaka, na sehemu ya mafuta yake, pamoja na ule ubani wake wote; ni kafara ya kusongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.